(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri leo ametembelea ujenzi wa Mnada wa Kisasa unaofadhiliwa na Maradi wa LIC (Local Investment Climate Project) unatarajiwa kutumia zaidi ya Tshs. 50,000,000/= mpaka kukamilika kwake. LIC imefadhili miradi mingi mikubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ikiwemo Ujenzi wa Mfereji wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Lumuma, Kituo cha Wanyamakazi Kibakwe na Kituo cha Biashara.
Katika mradi huu wa ujenzi wa Mnada wa kisasa unajumuisha ujenzi wa zizi la mbuzi na ng'ombe, pakilio la ng'ombe na machinjio. Kwa sasa zizi limeshakamilika ila pakilio na machinjio bado yapo katika hatua za ukamilishaji ambapo jengo la machinjio lipo katika hatua ya lenta.
Mazizi ya Ng'ombe na Mbuzi
Afisa Mifugo na Uvuvi wa wilaya Ndug. Godfrey Ayako anaeleza namna ya mnada huu utakavyoweza kuhudumia wananchi wa Mpwapwa kwa kupata fursa za kibiashara kama vile biashara ya nyama, pombe, vyakula, nguo na matunda. " Wananchi watapata ajira za muda na kudumu ambapo ajira za ulinzi na usafi zitapatikana hapa. Vile vile katika zizi la ng'ombe kutakuwa na pakilio ambapo wanunuzi wa ng'ombe wanaweza kupakia mifugo hiyo na kusafirisha, hivyo kupitia biashara zote zitakazokuwa mnadani hapo Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa itakusanya mapato ya ushuru wa mifugo na biashara ndogo ndogo".
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimeri (wa kwanza kushoto mstari wa mbele) akitoa maelekezo juu ya ujenzi wa shimo la maji taka katikamachinjio
Aidha Mkuu wa Wilaya Mhe. Shekimweri amepongeza mradi huu kuwa unaenda vizuri na kamati ya ujenzi imemhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa kazi wataikamilisha mapema iwezekanavyo kwa kuwa vifaa vyote vya ujenzi vipo.
Kufuatia kauli ya kamati ya ujenzi, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa ameiagiza kamati ya ujenzi kukamilisha mradi huu tarehe 15 Februari 2019 ambapo pia Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Mahenge atakuja kutembelea mradi huu hivyo kasi iongezwe. Pia ameongeza kuwa kama tutafanya mradi huu vizuri LIC watatufadhili miradi mingine kama vile Mnada wa Chipogoro, Rudi na Msagali.
Vile vile Mhe. Shekimweri amempongeza Ndug. Ayako kwa usimamizi mzuri wa mradi huu na ametoa wito kasi na nguvu hii ya ujenzi wa mnada iwekwe pia katika ukamilishaji wa ujenzi wa soko la Mji Mpya.
Mkuu wa Wilaya amehoji kama eneo linalojengwa mnada ni la mtu binafsi au la kijiji na kama lina hati, akitolea ufafanuzi Afisa Ardhi na maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Anderson Mwamengo kuwa kisheria eneo hili ni la kijiji kwa kuwa lilikuwa halitumiki kwa muda wa miaka 12 hivi na limeota uoto wa asili, na pia ni eneo lililopo ndani ya kijiji cha Ilolo.
Nae, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. George Fuime ambaye pia ni diwani wa kata ya Mpwapwa Mjini ametoa neno la shukurani kwa kuipongeza kamati ya ujenzi kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa mnada huu na kumpongeza Mkuu wa Wilaya kwa ufuatiliaji wa mara kwa mara.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.