Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa Dc
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndugu Paul Mamba Sweya leo amemualika Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Alinanuswe Mwakiluma akiwa na timu yake ya Wasanifu wa Majengo na wahandisi kuja kukagua Jengo la Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambalo ujenzi wake ulikoma tangu mwaka 2014.
Kihistoria Jengo la Ukumbi wa Halmashauri ya Mpwapwa lilianza kujengwa tarehe 28 Machi 2013 kwa mujibu wa Mkataba namba LGA/023/CDG/W/QT/2012/13/01 na Kampuni ya Magoma & Lyatimbo Construction LTD ya Dar ES Salaam kwa thamani ya Tsh. 356,500,000/= hadi jengo kukamilika. Jengo hilo kama lingekamilika lilitakiwa kuwa na Ukumbi wa mikutano, Ofisi za Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkamamu mwenyekiti wa Halmashauri na Mwandishi wa Mikutano ya Halmashauri.
Jengo la Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa lilipoishia tangu Mwaka 2014 Hadi sasa.
Dhumuni la kuwaita wataalam toka TBA ni kuja kupima na kutathmini kama jengo hilo bado lina uwezo wa kuendelezwa kujengwa ili Halmashauri ya Willaya ya Mpwapwa iendelee kujenga au kama lina kasoro, hivyo libomolewe na ujenzi uanze upya.
Akizungunza katika Utambulisho wa wataalam hao Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndugu Sweya, amesema "Tumewaita hawa wataalam ili waje kupima na kutushauri kwa maandishi kama tunaweza kuendelea na ujenzi au jengo halina nguvu ya kuhimili muendelezo wa ujenzi kwa kuwa jengo hilo lilijengwa muda mrefu na halikumaliziwa tangu mwaka 2014 mpaka sasa, hivyo Halmashauri ya Wilaya imeona ipo haja ya kumalizia ili tuwe na ukumbi wa kisasa hata Viongozi toka Makao Makuu ya Nchi Dodoma siku moja waweze kufanyia vikao vyao Mpwapwa ". Ndugu Sweya ameongeza kuwa "Hapa Mpwapwa hakuna Ukumbi wa Kisasa hivyo kumalizika kwa ukumbi huu utawezesha upatikanaji wa mapato kwa kukodisha kwa ajili ya sherehe na mikutano ya jamii".
Timu ya Wataalam toka TBA na Halmashauri wakikagua Jengo la Ukumbi (Wakwanza Kushoto - Mhandishi Mwakiluma toka TBA na Wapili Kushoto - Ndugu Paul Sweya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa)
Nae, Kaimu Mkurugenzi wa TBA Mhandishi Mwakiluma amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpwapwa kwa kuchukua jitihada za kutaka kumalizia jengo hili, na amekiri kuwa jengo ni la muda mrefu na wamekuja na kifaa maalau kinachojulikana kwa jina la kitaalam kama Rebound Hummer kwa ajili ya kupima ubora wa jengo katika maeneo muhimu kama kwenye nguzo na bim ili kubaini kama jengo bado lina uwezo wa kuhimili mwendelezo wa ujenzi.
Mhandisi Mwakiluma amesema "Kazi ya leo ni kupima tu na kuchukua data toka katika kifaa maalam ndio maana mnaona hapa tunapiga kama risasi katika maeneo ya nguzo na bim baada ya zoezi hili tutawaletea taarifa ya maandishi ambayo ndio itaamua kama jengo lote libomolewe au ujenzi uendelee ".
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndugu Sweya (kulia) akiwaonyesha wataalam maeneo ya Jengo la Ukumbi huo
Baada ya zoezi la kukagua jengo na kuchukua vipimo kukamilika Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpwapwa ameishukuru Timu nzima ya TBA kwa kuitikia wito na kuja kufanya kazi hii nzuri kwa ushirikiano mkubwa.
****Mwisho****
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.