(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabari Shekimweri ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kituo cha Afya Kibakwe katika hatua ya umaliziaji. Katika ziara ya leo amekagua madirisha, milango, masinki ya kunawia maji, umaliziaji wa plasta katika baadhi ya majengo, umaliziaji wa vigae vya sakafuni (tiles) na umeme. Akipongeza hatua iliyofikiwa kwa sasa Mhe. Shekimweri amesema "katika ziara yangu ya tarehe 31 Desemba, 2018 nilibaini mapungufu kadha na nilitoa maagizo ambayo yametekelezwa, hivyo nimeridhishwa na hatua hii".
Pia Mkuu wa Wilaya ametoa agizo kuwa jengo la kuhifadhia maiti halina milango, hivyo ifungwe mara moja na Alhamisi tarehe 10 Januari, 2019 iwe mwisho.
Jengo la Wodi ya Wazazi katika Kituo cha Afya Kibakwe Ambalo lipo katika hatua za mwisho kukamilishwa
Katika hatua nyingine Mhe. Shekimweri ameridhishwa na hatua ya ukamilishaji wa miundombinu ya umeme katika nyumba ya mganga ambapo katika ziara yake iliyopita alitoa siku tano kwa Fundi Umeme Ndug. Michael Lubaja kukamilisha kazi hii na fundi alikamilisha kama alivyoagizwa. Kukamilisha kazi hii kwa wakati imesababisha Mkuu wa Wilaya kufurahi na kuomba wajumbe waliohudhuria kumpigia makofi ya sifa fundi umeme huyo kwa kukamilisha kazi iliyobaki ndani ya siku tano.
Jengo la Nyumba ya Mganga katika Kituo cha Afya Kibakwe Ambalo lipo katika hatua za mwisho kukamilishwa
Kwa upande mwingine, katika mradi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Kibakwe ambapo kwa sasa yapo katika hatua ya madirisha. Katika hatua hii Mkuu wa Wilaya amesifu kasi inayoendelea na kusitisha wazo lake alilotoa katika ziara ya awali kuwa angeliwaleta Askari wa JKT kuja kusaidia kazi ya ujenzi wa madarasa kwa kuwa kasi ya ujenzi ni ya kusuasua. Hata hivyo Fundi mkuu wa ujenzi wa madarasa na kamati yake ya ujenzi wamejipanga vizuri katika kuhakikisha wanaenda kwa kasi kwa kufuata ubora na viwango vilivyoaanishwa.
Mkuu wa Wilaya amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Paul Mamba Sweya kuhakikisha madirisha, milango, mbao na bati zinaandaliwa mapema katika ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Kibakwe ili kazi hii isisimame kwa kukosa vifaa.
Aidha ziara ya Mkuu wa Wilaya ilielekea Kata ya Gulwe ambako kunajengwa shule ya Sekondari Gulwe kwa nguvu za wananchi kwa kuhamasishwa na viongozi wa kata hiyo akiwemo diwani kwa kufyatua tofali, kusomba mchanga, maji , mawe, na kujitolea maeneo ya kujenga shule. Pia wamewahamasisha wananchi wachangie fedha ambapo mpaka sasa Shilingi Milioni Kumi na elfu themanini na mbili tu (Tsh.10,082,000/=).Ujenzi kwa sasa umefikia katika hatua ya madirisha na unaendelea ambapo madarasa matatu yamefikia hatua ya lenta ambapo jengo moja lenye madarasa limefikia hatua ya madirisha.
Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gulwe
Mkuu wa Wilaya ameagiza kuwa ili kutatua migogoro ya ardhi wananchi waliotoa aridhi kwa ridhaa yao kuwe na makubaliano ya maandishi, eneo hili la shule lipimwe na liwe na hati. Mkuu wa Wilaya ameuliza kama wasimamizi wa ujenzi wa shule wamejiridhika kama majengo hayapo katika hifadhi ya barabara, Mwenyekiti wa kijiji amejibu kuwa wataalam wamejiridhisha kuwa majengo hayapo katika hifadhi ya barabara.
Mhe. Shekimweri amewapongeza sana viongozi wa kata pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kujitoa kwa ajili ya kuanziasha ujenzi wa shule ya sekondari ya Gulwe baada ya kuona watoto wao wanasoma kata za mbali ikiwepo Mazae, Vinghawe na Mpwapwa Mjini. Tunaomba viongozi muendelee na hamasa kama hii, amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.