(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amezindua Kampeni ya Ugawaji wa Vyandarua kwa kaya bila malipo, zoezi litakalofanyika kwa Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa. Kikao hicho cha uzinduzi kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kikihudhuriwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, waratibu wa ugonjwa wa malaria toka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mkoani Dodoma, Kongwa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama kutoka katika Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa.
Katika hotuba yake Mkuu wa Wilaya amesema "Siku ya leo tutapitishwa na kuelekezwa hali ya malaria katika Nchi yetu na tutapata uelewa mpana wa malaria. Ugonjwa huu ndio unaongoza kwa kwa kusababisha vifo vingi kuliko hata ukimwi na magonjwa mengine".
Wajumbe Akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mhe. Shekimweri (waliokaa mbele, wa pili kulia) wakiwa katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa wakifuatilia maelekezo ya kikao cha maaandalizi ya kampeni ya ugawaji wa vyandarua mara baada ya uzinduzi.
Vilevile katika hotuba yake Mhe. Shekimweri amesema "Katika ripoti ya Dunia ya Malaria ya mwaka 2018, inaonesha kulikuwa na wagonjwa wa malaria milioni 219 na wanaokufa ni 435,000 duniani kote, kati ya wagonjwa hao, wagonjwa 91% na vifo 90% kutoka Afrika. Hii ina maana kuwa bara la Afrika hali sio nzuri hivyo ndio maana Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli amechukua hatua ya kugawa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu kwa kaya. Hivyo nasi tuliopo hapa katika shughuli hii tuchukulie uzito mkubwa mkutano huu ili kuthibiti malaria". Pia ameongeza kuwa katika nchi 10 za Afrika ikiwemo Tanzania na India zinachangia zaidi ya 70% ya wagonjwa wa malaria.
Vile vile Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa timu itakayohusika na kazi ya ugawaji wa vyandarua kuwa makini na kuzingatia wajibu wao, kutkana na maelekezo ya majuku ya kazi na ratiba ya kazi. Angalizo mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo wahusika katika kazi hii mnatakiwa kuwa makini ili kusitokee malalamiko kwa wananchi yatakayosababisha madhara katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Pia Mkuu wa Wilaya ametoa ushauri kwa wadau wa Program ya Taifa ya Kuthibiti Malaria (National Malaria Control) iwe Program ya Taifa ya Kuzuia na Kuthibiti malaria (National Prevention and Control Program); kwa kuweka kipengele cha kuzuia kutasaidia kutokomeza mbu wasizaliane na kuua mbu katika mazalia yao na hivyo kutokomeza ugonjwa wa malaria.
Lengo la kugawa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu ni kutomeza Ugonjwa wa malaria ifikapo mwaka 2030 ambapo jumla ya vyandarua 414,579 vitagawawi kwa kaya za wilaya mbili, yaani kwa Halmashauri ya Mpwapwa 204,221 na Kongwa 210,358.
Aidha katika mafunzo hayo imeelezwa kuwa wananchi watapewa taarifa kuhusu uwepo wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua na zoezi la kujiandikisha kupitia maafisa watendaji wa kata na vijiji ili waweze kujitokeza kujiandikisha ili baadae wapatiwe vyandarua.
Mwisho mkuu wa Wilaya ya mpwapwa amewashukuru wageni wote waliohudhuria na kuwasisitiza kufanyiakazi maelekezo yote waliyopewa kwa umakini mkubwa ili kunusuru afya za kaya zilizohatarini katika ugonjwa wa malaria.
*****Mwisho*****
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.