(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri leo amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho kwa wajasiliamali vilivyotolewa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kuwagawia wafanyabiashara wadogo wadogo (wajasiliamali) ili waweze kutambulika. Uzinduzi huo umefanyika katika Ukumbi wa Jumba la maendeleo la Kata ya Mpwapwa Mjini katika Wilaya ya Mpwapwa.
Katika uzinduzi huo umehudhuriwa na Diwani wa kata ya Mpwapwa Mjini Mhe. George Fuime kama mwenyeji katika eneo lililofanyika uzinduzi huo, wajasiliamali zaidi ya 200 wa Mpwapwa Mjini, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Meneja wa TRA tawi la Mpwapwa, Wataalam toka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa pamoja na wafanyabiashara wakubwa wa maduka na mzao aikwepo Ndug. Lekime kwa lengo la kupata elimu juu ya ugawaji na matumizi ya vitambulisho hivyo.
Wajasiliamali wakisikiliza kwa umakini maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri katika Uzinduzi wa Vitambulisho vya Wajasiliamali katika Ukumbi wa Jumba la Maendeleo la Kata ya Mpwapwa Mjini.
Kwa upande wa Wilaya ya Mpwapwa idadi ya vitambulisho vilivyopokelewa toka Ofisi ya Mkuu wa Mkoani Domoma ni 3,500. Kwa mkoa wa Dodoma jumla ya vitambulisho vilivyopokelewa ni 25,000 ambapo kwa Wilaya ya Mpwapwa imepata vitambulisho 3,500 kuanzia Kitambulisho namba T00071501 hadi T00075000 vya awali kwa maana kama kuna idadi kubwa ya wajasilimali itaongezeka na vitambulisho vitaongezwa. Katika uzinduzi huu wa leo Mkuu wa Wilaya amegawa vitambulisho 8 kwa wajasiliamali 8 kama vitambulisho vya awali na vingine vitagawiwa kwa utaratibu uliopangwa na kikosi kazi.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri ametoa Masharti ya kupata na matumizi kitambulisho cha Mjasiliamali kwa wajasiliamali kama ifuatavyo:-
1. Hakikisha huna huna namba ya malipo ya kodi ya Mapato (TIN), na kama unayo na huitumii kulipa kodi waone TRA kwa utambuzi zaidi.
2. Hakikisha kuwa hujawahi kusajiliwa katika mfumo wa TRA au kulipia mapato TRA.
3. Hakikisha unajiandikisha kwa mtendaji wa Kata yako ili usajiliwe na unajaza fomu ambazo zinatolewa bure.
4. Matumizi ya kitambulisho ni mwaka mmoja tu, hivyo baada ya mwaka mmoja unatakiwa kuhuisha au kuingia kulipia TRA kama biashara yako itakua na kupata mauzo zaidi ya shilingi Milioni nne (Tsh. 4,000,000/=).
5. Kitambulisho kitatumika kwa mjasiliamali aliyesajiliwa na sio vinginevyo.
6. Hakikisha mauzo yako kwa mwaka hayazidi Tsh 4,000,000/= (Milioni nne).
7. Kitambulisho kimoja kitapatika kwa bei ya Tshs. 20,000/= na italipiwa benki ya NMB kwa akaunti namba 50410004258 NMB Benki na jina ni DAS Imprest Account.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (wapili kulia) akihutubia wajasiliamali Wilayani Mpwapwa katika Ukumbi wa Jumba la Maendeleo wakati wa Uzinduzi wa Vitambulisho vya Wajasiliamali.
Pia Mkuu wa Wilaya ametoa maelekezo kwa Kikosi kazi kinachoratibu utaratibu wa kugawa vitambulisho kwa wajasiliamali kama ifuatavyo:-
1. Kila mjasiliamali anayehitaji asajiliwe na kisha baadae kuchambua kama amekidhi vigezo na hajakidhi basi sababu ya kutokidhi iwekwe wazi na iandikwe.
2. Kamati ihamasishe na kuelimisha zaidi ili wajasiliamali wote wapate taarifa na kuweza kununua vitambulisho hivyo, mpaka leo ni vitambulisho 47 tu vimelipiwa.
3. Amewaagiza kuwa fomu zinatolewa bure
4. Kila kitambulisho bei yake ni Tsh 20,000/= tu.
5. Ili kupata kitambulisho lazima uwe na nakala ya kitambulisho chako kama cha kura au utaifa au kazi, barua ya serikali ya mtaa, leseni ya udereva, hati ya kusafiria.
6. Fedha ya kitambulisho cha mjasiliamali ilipwe kwenye akaunti namba 50410004258 NMB Benki na jina ni DAS Imprest Account.
7. Katika mchakato wa kugawa vitambulisho lifanywe kwa uadilifu na uaminifu mkubwa kusiwe na rushwa na hongo.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (watatu kushoto) akikabidhi kiatambulisho kwa mmoja wa wajasiliamali wilayani Mpwapwa katika Ukumbi wa Jumba la Maendeleo
Aidha Mkuu wa Wilaya Mkuu wa Wilaya ametoa angalizo kwa Kikosikazi kinachoratibu utaratibu wa ugawaji wa vitambulisho vya wajasiliamali kama ifuatavyo:-
1. Asitokee mfanyabiashara akaigawa biashara kwa ndugu au marafiki zake ili biashara iwe ndogo ili kupata kitambulisho atachukuliwa hatua za kisheria.
2. Pia ametoa wito kuwa kama kutakuwa na udanganyifu wowote utakaofanywa na wafanyabiashara taarifa itolewe mapema ili tuchuke hatu.
3. Pia amewasihi wajumbe wa kikosikazi wawe wawazi katika kutoa taarifa au kuuliza mambo ambayo yanahitaji ufafanuzi zaidi.
4. Amewasisitiza wajasiliamali wote waombe hata kama wana TIN ili kikosi kazi kichambue.
Kwa Upande wao Wajasilimali wa Wilaya ya Mpwapwa wamemuomba Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri awafikishie shukurani zao za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali wafanyabiasha ndogo ndogo kwa kuwa hapo awali walikuwa wanasumbuliwa sana na maafisa biashara toka Halmashauri na viongozi wa mamlaka ya kodi ya mapato (TRA). Kwa sasa, vitambulisho vitakuwa ufumbuzi na tutafanya biashara kwa utulivu kwa mwaka mzima. alisema mmoja wa wajasiliamali.
Moja ya vitambulisho vilivyogawiwa kwa wajasiliamali Wilayani Mpwapwa
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.