Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa yaazimisha siku ya Mtoto Afrika leo tarehe 16 Juni 2018. Maazimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Lupeta kata ya Lupeta wilayani Mpwapwa ambapo wananchi wote, wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo wamehudhuria. Katika maazimisho hayo mgeni rasmi ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mpwapwa Ndg. Maria P. Leshalu akiambatana na wakuu wa idara pamoja na baadhi ya waheshimiwa madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
Siku ya Mtoto Afrika hufanyika kila mwaka katika Bara zima la Afrika ikiwa ni kumbukumbu ya kuwaenzi na kuwakumbuka watoto waliohangamia kwa kuteswa na kuuawa katika kitongoji cha SOWETO huko Afrika Kusini baada ya kuandama kudai haki zao katika serikali ya kikaburu. Siku hiyo ilianza kuazimishwa baada ya Umoja wa Mataifa kuridhia kupitisha Mkataba wa Kulinda Haki za Watoto tarehe 20 Novemba 1989.
Mgeni rasmi Ndg. Maria P. Leshalu (wa tatu toka kushoto aliyesimama) ambaye ni kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa akihutubia siku ya Mtoto Afrika. (Picha Na: Shaibu Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Katika hotuba yake mgeni rasmi amewapongeza wadau mbalimbali kwa kusema, "Napenda kuwapa hongera wale waliojaliwa kujinyima na kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani naomba Mola awaongezee thawabu. Aidha, napenda kuwashukuru sana na kuwapongeza ninyi nyote mlioitikia wito wa kufika hapa siku hii ya leo, tunawapongeza jinsi ambavyo mmeandaa Maadhimisho ya siku ya Mtoto katika Wilaya yetu hii ya Mpwapwa, mlivyoweza kushiriki nyinyi pamoja na watoto wetu, hivyo nawapongezeni sana. Shukrani za kipekee ziwaendee Shirika lisilo la Kiserikali la Compassion kupitia Makanisa ya TAG, KKKT, Mt. Paul, EAGT Sayuni na Kanisa la Watakatifu wote na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (Children’s Dignity Forum). Aidha, napenda kutoa shukrani kwa Benki za NMB, CRDB Mpwapwa na Wafanyabiashara kwa michango yao na kuwezesha kufanikisha maadhimisho ya siku ya leo. Nimefurahi pia kupata nafasi hii ya kuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho haya ya siku ya Mtoto wa Afrika yanayoadhimishwa kiwilaya hapa leo Kata ya Lupeta. Lakini pia nimefurahi kuona maonyesho, shughuli za vipaji mbali mbali vya watoto zikiwemo nyimbo, maigizo Sarakasi na Mashairi. Nawapongeza sana kwa wale watoto walioonesha vipaji vyao na natoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya kuendelea kuvilea, kuviendeleza na kuvikuza vipaji hivi ili baadae watoto pamoja na Taifa letu liweze kunufaika na vipaji hivi. Aidha, nimesikia Risala ya watoto ambayo imejumuisha haki za kimsingi za watoto ambayo imebainisha wazi changamoto wanazopitia watoto wetu zenye kukatisha ndoto zao lakini pia yenye kutoa majukumu ya kila mdau yaani wazazi/walezi, familia, taasisi za dini, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla katika kukabiliana na changamoto hizo."
Wanafunzi wakionyesha bidhaa mbalimbali walizotengeneza katika maazimisho ya Siku ya Mtoto Afrika wilayani Mpwapwa (Picha Na: Shaibu Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Pia akiendelea kuhutubia mgeni rasmi ameeleza kwa ufupi madhumuni ya kuadhimisha siku hii ya Mtoto wa Afrika tarehe 16 Juni kila mwaka. Siku hii huadhimishwa na nchi huru za bara la Afrika, Tanzania ikiwa ni mojawapo. Madhumuni ya kuadhimisha siku hii, kwanza ni kumbukumbu ya Mateso na Kunyanyaswa kwa watoto wa kitongoji cha Soweto huko Afrika ya kusini wakati wa Utawala wa Kikaburu, siku ambayo watoto wa Soweto waliandamana kupinga Sheria mpya ya Makaburu katika kufundisha shule zote kwa lugha ya kigeni. Siku hiyo watoto waliandamana kwa nia ya kusikilizwa shida zao. Matokeo yake Askari wa Makaburu waliamriwa kuwatawanya kwa nguvu. Katika kufanya hivyo walifyatua risasi na kuwauwa watoto wengi. Jambo ambalo ni ukatili kwa watoto. Lakini pia ni fursa kwetu kukaa chini na kutafakari juu ya hali ya ulinzi pamoja na ustawi wa watoto wetu kwani watoto ni nguzo imara ya jamii yoyote iliyoendelea.
Kila Mwaka maadhimisho haya huambatana na kauli mbiu zenye lengo la kuunganisha nguvu za pamoja katika kukuza ustawi wa mtoto. Kauli mbiu ya mwaka huu kwa bara la Afrika inasema “TUSIMWACHE MTOTO NYUMA” na kwa kuwa nchi yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dr John Pombe Magufuli imedhamiria kuingia kwenye uchumi wa Viwanda, Kauli mbiu yetu kwa Tanzania inasema “KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA; TUSIMUACHE MTOTO NYUMA”
Kimsingi Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania ya Mwaka 2008 na Sheria ya mtoto namba 21/2009 zimetungwa na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano na kusainiwa na Mheshimiwa Rais. Lengo hasa la utungwaji wa Sera na sheria hizi ni kuwezesha ulinzi wa kijamii na kisheria kwa watoto na kusaidia mifumo rasmi yenye kutekeleza na kusimamia haki za mtoto kuweza kutoa haki na kutekeleza sheria ipasavyo ikiwemo haki ya kuendelezwa.
Awamu ya tano ya mfumo wa Utawala nchini imekuwa na msisitizo mkubwa wa kujenga uchumi wa kati ambao msingi wake ni maendeleo ya viwanda. Msisitizo huu umelenga katika kuanzisha viwanda vidogo vya Kati na vikubwa vya uzalishaji wa bidhaa katika ubora unaotakiwa. Viwanda vingi havina budi vitokane na kazi za mikono za kiufundi kama vile ususi, uchoraji, uashi, uchomeaji na uyeyushaji wa malighafi za asili ya chuma. Pia usindikaji wa malighafi za kilimo na ufugaji kama vile matunda, mboga mboga, nafaka, maziwa, nyama, na mayai.
Watoto wakiimba shairi katika maazimisho ya Siku ya Mtoto Afrika mbele ya mgeni rasmi wa maazimisho hayo. (Picha Na: Shaibu Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Wataalamu wa elimu wamekuwa na mijadala mbalimbali kuhusu ni kwa kiwango gani mifumo yetu ya elimu rasmi inavyoweza kuchangia malengo hayo. Wamekuwa wakiangalia pia uwezo wa wasomi wetu wanaozalishwa na taasisi zetu za elimu ni kwa kiwango gani wana uwezo wa kufanikisha kufikiwa kwa Tanzania ya Viwanda.
Pia wataalamu wa saikolojia ya Jamii nao wameeendelea kushauri ni kwa kiwango gani malezi na makuzi yetu yanahitajika kujikita katika kubaini na kuviendeleza vipaji vya ubunifu lakini pia kujenga uthubutu kwa vijana wetu kuanzisha viwanda vidogo na kujihusisha na uzalishaji. Makundi yote hayo yana lengo moja la kuhakikisha yanatoa mchango wao katika kukuza uchumi na hali za maisha ya wananchi kiuchumi, kimaadili, kisiasa na kiutamaduni.
Uendelezwaji wa WatotoZipo sababu za kibaiolojia, kimazingira na mifumo ya tamaduni za kijamii inavyoathiri maendeleo ya watoto na vijana kufikia kujiamini na kuthubutu kuchangia maendeleo ya kaya na taifa kwa ujumla ili Tupate Vijana Wenye Vipaji.
Malezi Miaka Mitatu hadi Sita Kipindi hiki ni muhimu kwa wazazi, walezi kuwapa watoto fursa za kucheza michezo mbalimbali. Jukumu la wazazi linapaswa kuwa ni kuhakikisha usalama wa kimazingira na kuwezesha katika vifaa vya kuchezea. Katika kipindi hiki watoto wanahitaji kucheza ikiwa ni pamoja na kucheza na marafiki, ni vyema wazazi wawaruhusu pasipo kuhofu kuchafuka kwani huwajengea afya bora ya mwili na akili. Watoto wana kawaida ya kutengeneza ratiba zao za michezo ambazo wakati mwingine ni tofauti kabisa na ufikiri wa watu wazima. Hivyo, wanapojitungia michezo yao, watu wazima wawape uhuru huo wa kucheza ikiwa ni pamoja na uwepo wa uangalizi wa wazazi au watu wazima ili kuhakikisha michezo iliyo hatari na yenye kuepuka maadili inaepukwa. Watoto wanapocheza katika mazingira ya shule au nyumbani wanakuza fikra na ndoto zao za maisha ya baadae. Ndoto hizo zinapaswa kukuzwa kwani huwawezesha kujenga picha ya ni kina nani wanataka wawe baadae katika jamii yao na Dunia kwa ujumla.
Familia nyingi na jamii kwa ujumla zimekuwa haziwekezi katika vifaa na viwanja vya michezo ya watoto. Kweli ni gharama lakini hatuna budi kufanya hivyo.
Malezi katika kipindi cha Miaka 6 hadi 11.
Kipindi hiki watoto wengi wamekuwa tayari wapo shuleni. Inafahamika kuwa shule ni wakala Mkubwa wa mabadiliko. Kuwepo kwa Sera ya elimu bure kumeongeza idadi ya watoto wanaoandikishwa katika ngazi ya elimu ya Msingi. Wajibu wa jamii uwe kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa, lakini pia jamii isisahau kuwezesha watoto hao katika mahitaji mengine muhimu shuleni kwa kushirikiana na uongozi wa shule na pia kuhakikishiwa ndoto zao za elimu hazikatishwi kwa sababu yoyote ikiwamo ndoa na mimba za utotoni. Shuleni wanafunzi wapewe fursa ya kushiriki michezo mbali mbali na kazi za sanaa na ubunifu. Tumeshuhudia idadi kubwa ya vijana wakitaka kushiriki katika shughuli za sanaa na uigizaji, uchekeshaji, uongozi wa sherehe na matukio, muziki na urembo.
Watoto wakisoma risala katika maazimisho ya Siku ya Mtoto Afrika mbele ya mgeni rasmi wa maazimisho hayo. (Picha Na: Shaibu Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Ni vyema pia mkazo ukawekwa katika shughuli zinazohusisha ufugaji, kilimo na elimu ya ujasiriamali. Hasa katika kipindi hiki ambacho Wilaya yetu imeweka mkazo katika kuanzisha zao la Korosho ambalo litakuwa mkombozi mkubwa kwa Uchumi wa Wilaya yetu ya Mpwapwa, ni muhimu kuendelea kuhakikisha wanajifunza kwa vitendo kupitia mashamba mfano ya shule juu ya uendelezaji wa zao hili la Korosho.Kwa kusema haya, Jamii inaposisitiza uanzishaji wa viwanda mbalimbali ni vema sasa ikawekeza kuanzia kwa watoto wetu ili kupata suluhu ya kudumu na isiyo ya kipindi kifupi. Msisitizo mkubwa uwekwe katika elimu ya Sayansi na ufundi, sambamba na kutengwa kwa maeneo ya viwanja vya Uwekezaji kwa vijana.
Mtoto ametafsiriwa katika kifungu cha 4(1) cha sheria ya mtoto kuwa ni mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka kumi na nane (18). Sheria imeainisha haki za mtoto ikiwa na maana stahili muhimu za mtoto kumuwezesha kufurahia, na kuendelea kwake kuishi. Zaidi, sheria imeainisha wajibu wa mtoto kwa familia, jamii na nchi yake. Kuna haki mbalimbali zinazomuhusu mtoto ikiwemo haki ya kuishi, haki ya kupata jina, haki ya urithi, haki ya kutobaguliwa, haki ya kuendelezwa, haki ya kutoa mawazo katika masuala yanayomgusa maslahi yake na haki ya ulinzi. Kifungu cha 8(1)-(2) kinatamka kuwa ni wajibu wa mzazi au mlezi anayeishi na mtoto kuweza kumtunza mtoto kwa kumpatia haki pamoja na mahitaji kama Chakula, Malezi ikiwa ni pamoja na makazi, matibabu na kupatiwa chanjo, elimu, uhuru, haki ya kucheza, kustarehe na kupumzika.
Kifungu cha 21 na 27 ndio vyenye kutoa wajibu wa kimalezi kwa waangalizi wa watoto na mameneja wa Taasisi zinazolea watoto kama Compassion na makao ya watoto kwa kuainisha majukumu yafuatayo:- kuhakikisha maendeleo ya mtoto yanafikiwa wakiwa chini yao kama kupata elimu na kuangaliwa vyema katika upande wa afya, kuwasiliana na wazazi juu ya maendeleo ya mtoto na Ulinzi wa mtoto kwa kipindi chote wawapo katika kituo. Sheria imeweka wajibu kwa jamii kwa kumtaka mwanajamii mwenye taarifa au ushahidi kuhusiana na mtoto ambaye haki zake zinakiukwa na mzazi, mlezi au ndugu au mtu yeyote kutoa taarifa kwenye Serikali za mitaa, vyombo vya dola au kupiga Simu namba 116 inayohusu huduma kwa mtoto Tanzania, huduma hii haina malipo yoyote. Wazazi tushirikiane katika kutoa taarifa kamili na sahihi kwa wale wote ambao wanawafanyia watoto vitendo viovu vikiwemo ubakaji
na ulawiti ili Serikali iweze kuwachukulia hatua Kali za Kisheria kwa watakaobainika.
Watoto wakionyesha bidhaa walizotengeneza wao wenyewe katika maazimisho ya Siku ya Mtoto Afrika mbele ya mgeni rasmi wa maazimisho hayo. (Picha Na: Shaibu Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Serikali za Mitaaa zina wajibu wa kulinda na kutetea maslahi ya mtoto katika eneo husika kupitia Afisa Ustawi wa Jamii. Serikali za Mitaa zitashirikiana na jeshi la Polisi katika kuwatafuta wazazi, walezi, na ndugu wa watoto waliotelekezwa kwa nia ya kuwapatia watoto malezi yaliyojengwa katika misingi bora. Wazazi na jamii wanalo jukumu la kuwalinda watoto kwa kuwazuia kushiriki kwenye maeneo ambayo yanaweza kusababisha vitendo viovu kufanyika ikiwemo vibanda vya kuonyesha Sinema, kufuatilia zawadi zinazotolewa kwa watoto kwa watu wasiofahamika na wazazi na walezi wa watoto, kuweka utaratibu mzuri na salama wa watoto kwenda na kurudi shule kwa maeneo au vijiji ambavyo shule zipo mbali na makazi ya wananchi ili kuwalinda watoto na watu wabaya wanaotumia umbali huo kuwatendea uovu watoto. Pia wazazi, Taasisi na jamii kwa ujmla wake ninawaomba kuendelea kuitikia wito wa Serikali na kila inapowezekana kujenga mabweni katika shule zetu za Sekondari ili kuwasaidia ulinzi kwa mtoto. Watoto walindwe ili waweze kutimiza ndoto zao na kufikia malengo yao. Wazazi tukumbuke kuwa toka miaka ya zamani mtoto ni wa wote hivyo ni jukumu letu kuendelea kumlinda kwa gharama zozote kwani “Mtoto wa Mwenzio ni Mwanao Pia”
Iwapo Mamlaka ya Serikali za Mitaa haitafanikiwa katika kupata wazazi wa mtoto basi itaelekeza suala hilo kwa Afisa Ustawi wa Jamii. Afisa Ustawi wa Jamii na Polisi ni lazima wafanye Uchunguzi ndani ya eneo la Mamlaka ya Serikali za Mitaa juu ya ukiukwaji wa haki za mtoto. Kutokana na Changamoto zilizoainishwa kwenye Risala ya Watoto nitoe mwito kwa Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na wadau wengine wanaohudumia watoto kuweza kuwajengea Miundombinu rafiki kwa watoto ili kuweza kuibua vipaji mbalimbali walivyonavyo ikiwemo kutenga Maeneo ya Michezo, Kuandaa matamasha ya Maonyesho ya kuibua vipaji, na Alama za Barabarani hasa maeneo ya Shule. Aidha, Halmashauri isimamie sheria za majengo kuhakikisha yanayotumiwa na Jamii yawe na miundombinu rafiki kwa watoto na watu wenye ulemavu ili waweze kupata huduma kwa urahisi zaidi.
Mwisho mgeni rasmi ametoa ushauri kwa wadau wote wazazi/walezi, jamii, Taasisi za dini, Asasi za kiraia, Serikali za Mitaa na vyombo vya dola kushirikiana kwa karibu, kwa pamoja tutaweza kutekeleza kauli mbiu ya KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA, TUSIMUACHE MTOTO NYUMA.
Kwa taarifa zaidi pakua nyaraka hii hapa chini: Taarifa ya Siku ya Mtoto Afrika - Mpwapwa Tarehe 16 Juni 2018.pdf
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.