(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa wameamua kutekeleza agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasani, Kwa wananchi wote Nchini kufanya mazoezi kila jumamosi wiki ya pili ya kila mwezi.
Wananchi hao wamejitokeza kwa wingi katika mazoezi yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Chazungwa yakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri ambaye amejitahidi kuwahamasisha wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi tangu agizo lilipotolewa.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri amewasisitiza wananchi wa Mpwapwa kufanya mazoezi kila siku wanapopata muda iwe jioni au asubuhi ili kujiimarisha kiafya. Pia aliwahamasisha wananchi kwa kila mtaa na kata kuunda Klabu ya Riadha (Jogging Clubs).
Aidha, baada ya Mkuu wa Wilaya kuhamasisha uundwaji wa klabu za riadha, mwitikio umukuwa mkubwa na mpaka sasa kuna klabu 12 hai, klabu hizo ni National jogging Club, Kikombo, Mwanakianga, Hazina, TTC, Mpwapwa Sec, Ilolo, Igovu, Mjini kati, Mji mpya, Majengo na Ng'ambo.
Katika mazoezi yanayofanyika kila mwezi katika Jumamosi ya wiki ya pili ya Mwezi kama agizo linavyosema, kumekuwa na walimu wa michezo na madaktari wakielimisha wananchi umuhimu wa kifanya mazoezi kiafya na namna ya kufanya mazoezi bila kuleta madhara kwa mtu.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri ametumia fursa hii ya mkusanyiko wa wananchi kuwaomba kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuleta maendeleo. Pia amewataka kufanya mazoezi ili kuwa na afya ili waweze kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo kilimo, biashara na kujitolea katika kuchangia nguvukazi katika miradi ya serikali katika maeneo yao.
Vilevile ameipongeza Shule ya Sekondari Mpwapwa kwa kuwa ya kwanza kimkoa kwa kufaulisha vizuri matokeo ya kidato cha sita kwa mitihani ya mwaka 2019. Hivyo amewataka walimu na wanafunzi kuendelea kuweka jitihada ili kuishikilia nafasi hii kwa miaka ijayo na hata kuwa wa kwanza kitaifa.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.